CRDB, Clouds Media Wazindua Kampeni ya ‘Tunaku-BUSTI’ Kuwezesha Wajasiriamali Kufikia Masoko ya Kimataifa

Dar es Salaam, Agosti 6, 2026 – CRDB Bank kwa kushirikiana na Clouds Media Group (CMG) wamezindua kampeni ya ‘Tunaku-BUSTI’ itakayowawezesha wanawake na wajasiriamali kupata mkopo maalum wa dola za Marekani 3,700 kwa ajili ya kushiriki safari ya kibiashara ya Twende Duniani nchini China na Uturuki.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CRDB Bank jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Matawi na Biashara wa CRDB Bank, Mussa Lwila, alisema ushirikiano huo unalenga kuwafungulia wafanyabiashara wa Tanzania fursa za kimataifa kwa kuwaunganisha na masoko, maarifa na mitandao ya biashara.
Lwila alisema kupitia kampeni hiyo, wajasiriamali watapata mkopo wa dola 3,700, ambapo dola 3,000 zitatumika kugharamia safari na dola 700 zitakuwa fedha za matumizi binafsi (pocket money), huku lengo likiwa kuondoa kikwazo cha mtaji wa kushiriki safari za kimataifa.
Alieleza kuwa mpango huo utawapa washiriki nafasi ya kujifunza namna biashara zinavyoendeshwa katika masoko ya dunia, kukutana na wadau wa kimataifa na kujenga ushirikiano utakaowawezesha kukuza biashara zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa Clouds Media Group, Sheba Kussaga, alisema kupitia Jukwaa la Malkia wa Nguvu, Clouds imeamua kwenda hatua zaidi ya kutoa tuzo kwa wanawake na sasa inalenga kuwapa maarifa na fursa za kimataifa.
“Kwa miaka 10 tumekuwa tukimsherehekea mwanamke kupitia Malkia wa Nguvu, lakini sasa tunataka kumpeleka duniani. Lengo si kupanda ndege pekee, bali kupanua fikra, kuongeza elimu na kufungua fursa zitakazomwezesha kufanya biashara katika soko la kimataifa,” alisema Sheba.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Malkia wa Nguvu, Liliane Masuka, alisema washiriki wa safari hiyo watanufaika kwa kujenga mitandao mipya ya biashara, kukutana na wasambazaji na kutembelea viwanda nchini China na Uturuki ili kujifunza teknolojia na mbinu mpya za uzalishaji.
Alisema kupitia ushirikiano huo, zaidi ya wanawake 100 wanatarajiwa kunufaika na uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni moja, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wa Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara za kimataifa.


All Categories
Recent Posts
Wafanyabiashara Watembelea Soko Kubwa la Fanicha na Vifaa mbalimbali Vya Mapambo – Foshan ,China
Wanawake Wafanyabiashara Chini ya TWCC Wawasili Nchini China.
+ 255 779 888 901
info@malkiawanguvu.co.tz